Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameorodhesha vitendo vya Russia nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na mauaji na kusababisha ulemavu wa watoto, katika ripoti ya kila mwaka ambayo huwataja wahusika wa ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto.
“Nimeshtushwa sana na idadi kubwa ya mashambulizi dhidi ya shule na hospitali na wafanyakazi wanaolindwa, na idadi kubwa ya watoto waliouawa na kufanywa vilema kutokana na vitendo vya vikosi vya Russia na vikundi vinavyomiliki silaha,” Guterres alisema katika ripoti yake, iliyotumwa Alhamisi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ripoti yenye kichwa “Watoto na Migogoro ya Kivita,” ambayo bado haijachapishwa rasmi, inawataja na kuwaaibisha wahusika wanaosajili, kuua, kulemaza au kuwateka nyara watoto, kuwafanyia ukatili wa kingono, kuwanyima msaada wa kibinadamu, au kushambulia shule na hospitali.
Mwakilishi maalum wa Guterres, Virginia Gamba, amepewa mamlaka na Baraza la Usalama, kufanya kazi ili kuzuia na kukomesha ukiukaji huo mkubwa. Katika ripoti hiyo, iliyoonekana na VOA, Umoja wa Mataifa ulithibitisha kuuawa kwa watoto 136 na kulemazwa kwa watoto 518 nchini Ukraine, kunakohusishwa na vitendo vya vikosi vya Russia, na vikundi vinavyoshirikiana navyo, kuanzia mwezi Januari hadi Desemba mwaka 2022.