Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha juu ya kuenea magonjwa mbalimbali huko Sudan.
Sudan imetumbukia katika mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na vikosi vya msaada wa haraka RSF vinavyoongozwa na Kamanda Muhammad Hamdan Daghalo tangu Aprili 15 mwaka huu.
Mapigano hayo yanajiri huko Khartoum na katika miji mingine ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo.
Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitabiri kuwa, idadi ya wakimbizi mwaka huwenda ikaongzeka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita kwa kuzingatia kuongezeka mivutano na mapigano kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya RSf katika wiki za karibuni.
Televisheni ya Sky News imeripoti kuwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa watu milioni 11 wanahitaji huduma za tiba haraka iwezekanavyo huko Sudan. WHO aidha limeeleza kutiwa wasiwasi na athari za mapigano huko Sudan zilizokwamisha utolewaji wa huduma za tiba kwa wanawake na mabinti nchini humo na kueleza kuwa,hadi kufikia sasa zaidi ya theluthi mbili ya hospitali katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano zimefungwa.
Shirika hili pia limetahadharisha kuhusu kuenea magonjwa ya kuambukiza kama vile homa ya matumbo na pia malaria huko Sudan na kuomba msaada wa kifedha wa dola bilioni 150 ili kukidhi mahitaji ya matibabu katika maeneo yaliyoathiriwa namapigano.
Tangu kuanza kwa vita hivyo miezi miwili iliyopita, pande hizo mbili zimeendelea kulaumiana kwa kusababisha vifo vya raia wa kawaida.
Tume ya Umoja wa Mataifa, inasema watu zaidi ya Elfu Mbili wameuawa mpaka sasa.
Maelfu ya watu wameendelea kuteseka, kwa kukosa mahitaji muhimu ya kibinadamu kama dawa na chakula, huku huduma muhimu kama maji na umeme zikikatwa.