Mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona anafikiria kustaafu, vyombo vya habari vya Brazil viliripoti, huku akisumbuliwa na maumivu makali yanayomlazimu kuchomwa sindano ili kucheza.
“Ni mbaya. Suarez ana uwezekano wa kuwekewa kiungo bandia,” Guerra aliwaambia wanahabari katika uwanja wa Gremio.
Rais Alberto Guerra, amefichua kuwa mshambuliaji wa Uruguay na Gremio Luis Suarez anakabiliwa na ugumu wa kurefusha maisha yake ya soka kutokana na ugonjwa wa goti unaojulikana kama osteoarthrosis.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa Gremio, Guerra alifichua uzito wa hali ya Suarez, akisema kuwa kuna uwezekano wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36 kufanyiwa upasuaji wa goti lake kwani mpaka sasa Suarez amedungwa sindano nyingi na dawa, lakini inaonekana anakaribia kufikia kikomo cha kile ambacho goti lake linaweza kustahimili, na hivyo kuacha mustakabali wake haujulikani.
Licha ya matatizo yake, Suarez bado anashiriki kikamilifu katika mazoezi na amejumuishwa katika kikosi cha Gremio kwa ajili ya mechi yao ijayo dhidi ya America-MG katika Serie A ya Brazil.
Fowadi huyo wa Uruguay, ambaye alijiunga na Gremio Januari na ana mkataba hadi Desemba 2024, alifanikiwa kufunga mabao 11 katika michezo 25 hadi sasa.
Suarez pia amekuwa akihusishwa na kuhamia klabu ya MLS Inter Miami, ambapo anaweza kuungana na Lionel Messi, rafiki yake wa karibu na mchezaji mwenza wa zamani.