Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mifumo ya kieletroniki katika ukusanyaji wa mapato, mazingira ya kufanyia kazi kwa ujenzi wa Ofisi za kisasa, upatikanaji wa vitendea kazi na utoaji wa mafunzo kwa watumishi ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo.
Ameyasema hayo leo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa umma Zanzibar na kuzindua mifumo mitatu ya kieletroniki ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-Wakili.
Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali italinda na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kila hali ya uchumi itakaporuhusu na kupandisha pencheni kwa wastaafu na tayari imeanza utaratibu mpya wa kulipa pencheni jamii kwa mwaka huu.
Tangu Serikali ya Awamu ya Nane ilipoingia madarakani jumla ya mifumo 28 ya kieletroniki imetengenezwa kwa kuongeza ufanisi katika uwajibikaji na utoaji wa huduma bora.
Mifumo mitatu imezinduliwa rasmi leo ikiwa ni pamoja na mfumo jumuishi wa taarifa za watumishi na malipo ambao utakuwa na mchango mkubwa wa uwekaji na uhifadhi wa taarifa za watumishi na kurahisisha mwenendo wa miamala ya fedha kwa kudhibiti wizi wa fedha za Serikali.
Vilevile mfumo wa Zan Ajira ni muhimu katika kurahisisha shughuli mbalimbali zinazohusu ajira na kuimarisha misingi ya usawa.
Aidha Rais Dk.Mwinyi ametoa wito kwa watumishi wote kuitumia mifumo yote iliyoanzishwa ili kuleta tija iliyokusudiwa na kuimarisha ufanisi katika Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi pia ameuhimiza uongozi wa wakala wa Serikali mtandao uongeze kasi katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma.
Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itaziimarisha Taasisi zote zinazoshughulika na usimamizi wa utawala bora ikiwemo ZAECA, CAG, DPP na Tume ya maadili kwa Viongozi wa umma kwa kuzipatia nyenzo na mafunzo ili ziweze kusimamia kwa ufanisi zaidi masuala yanayohusu uwajibikaji, uadilifu, uwazi, upatikanaji wa haki na huduma bora kwa wananchi na kutunga sheria mpya zinazohitajika ili kuzipa nguvu zaidi taasisi hizo.