Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani Jijini Arusha leo June 25,2023 ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni kwamba ana matumaini maboresho yanayoendelea kufanywa katika Bandari za Tanzania yatajumuisha ufungaji wa mitambo ya kisasa itakayosaidia kubaini shehena zinazopitishwa zikiwa na dawa za kulevya ndani yake.
“Bandari zetu ni milango ya kuhudumia usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwenda Nchi jirani inawezekana baadhi ya Wahalifu wakatumia usafirishaji wa shehena hizo kupitisha dawa za kulevya na ndio sababu ninasisitiza umuhimu wa kubadilishana taarifa za kiitelejensia na Nchi jirani na kufanya kazi kama Nchi moja baina ya Tanzania bara na Zanzibar kwasababu milango hii Zanzibar ipo wazi sana Mtu akitoka Duniani anaweza kuingia njia yoyote Zanzibar na kutoa Zanzibar kuleta Bara ni kazi rahisi”
“Tushirikiane kuongeza mapambano ya kudhibiti dawa za kulevya, ni matumaini yangu maboresho yanayoendelea kufanywa katika Bandari zetu yatajumuisha ufungaji wa mitambo ya kisasa itakayosaidia kubaini shehena zinazopitishwa zikiwa na dawa za kulevya ndani yake”
“Hata hivyo kuwa na mitambo ni jambo moja lakini kuwa na Watendaji waadilifu ni jambo la pili, tukiwa na mitambo bila Watendaji wenye uadilifu hatutopata matokeo tunayoyatarajia, tunahitaji Watumishi wenye uzalendo wanaoweka mbele maslahi ya Taifa, Watumishi wa Bandari, wa TMDA, wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya wote tutangulize maslahi ya Taifa mbele ndipo tutashinda vita hii”