Kabila alikumbusha kwamba yeye na muungano wake wa kisiasa hawatashiriki mchakato wa uchaguzi kabla mchakato huo kutimiza masharti ya uchaguzi bora.
Joseph Kabila alikuwa amebaki kimya kwa muda mrefu baada ya kuacha madaraka Januari 2019 kwa mrithi wake Felix Tshisekedi.
Kimya hicho kiliwafanya wengi kufikiria kwamba raïs huyo wa zamani amestaafu kisiasa.
Lakini siku chache zilizopita, miezi sita kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi wa Desemba mwaka huu, Kabila alikutana na viongozi wa FCC ambao ni muungano wa vyama vinavyomuunga mkono na kuwaahidi kuwa atazidisha mikutano na wale ambao wamebaki waaminifu kwake. Miongoni mwa wale walioshiriki mkutano huo ni Ferdinand Kambere, Naibu Katibu Mkuu wa PPRD, chama cha Joseph Kabila.
Upande wake, Denis Kadima, Kiongozi wa tume huru ya uchaguzi, ametoa wito kwa mchango wa wote ili kufikiria mchakato wa uchaguzi utakaoaminika.
Joseph Kabila anadai masharti yote ya kufanyika uchaguzi bora kutimizwa na bila hayo, basi yeye na wafuasi wake hawatashiriki mchakato wa uchaguzi huo.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajiandaa kufanya chaguzi nne Desemba 20. Nazo ni uchaguzi wa rais, ule wa wabunge wa kitaifa na wa mikoa, pamoja na chaguzi za manispaa.