Nchini Mali, raia walipiga kura kuidhinisha rasimu ya katiba mpya katika zoezi lililofanyika tarehe 18 ya mwezi Juni ambapo asilimia 97 ya wapiga kura waliunga mkono mchakato huo kwa mujibu wa tume ya uchaguzi katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Kwa mujibu wa utawala wa kijeshi nchini humo, hatua hiyo sasa inatoa nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwezi Februari mwaka ujao, hatua itayorejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia.
Mkuu wa tume ya uchaguzi Moustapha Cisse amesema chini ya asilimia 40 ya wapiga kura kati ya 8.4 ndio waliojotekeza kushiriki zoezi hilo.
Mali imeshuhudia mapinduzi mawili ya kijeshi tangu mwezi agosti mwaka wa 2020 wakati utawala wa rais Ibrahim Boubacar ulipoangushwa.
Kiongozi wa kijeshi ambaye pia ni rais wa mpito Assimi Goïta alisema katika hotuba yake kwamba “anashawishika kwamba kura hii ya maoni inafungua njia kwa Mali mpya, yenye nguvu, yenye ufanisi na inayoibukia, lakini zaidi ya yote Mali katika huduma ya ustawi wa watu”.
Mabadiliko hayo ya katiba pia yanaitaja Mali kama taifa lisilo na dini, hatua iliyopingwa na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu.