Kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20 Wagonjwa wapya watatu wa malaria wamegundulika Nchini Marekani huku Mgonjwa mmoja akitokea katika jimbo la Texas na wawili wakiwa katika jimbo la Florida ambapo kilichosababisha gumzo zaidi na hofu ni kwamba Wagonjwa hawa watatu hawakuwa wamesafiri kwenda nje ya Nchi.
Rekodi zinaonesha kuwa mara ya mwisho Marekani kuwa na kisa cha Malaria ilikua ni mwaka 2003 katika Kaunti ya Palm Beach, Florida ambapo visa vyote vya ugonjwa wa malaria vilivyogundulika kwa miaka ya nyuma vilitoka kwa Watu waliosafiri kwenda nje ya nchi ambako walishambuliwa na mbu wanaoeneza malaria.
Inaaminika kuwa Wagonjwa hawa watatu wanaweza kuwa waliopata maambukizi baada ya kung’atwa na mbu aliyeng’ata Msafiri aliyebeba ugonjwa huo na kurudi nao Marekani.
Sehemu kubwa ya bara la Afrika na maeneo mengine kama Asia ya Kusini, Visiwa vya Carribean, Asia ya Kusini-Mashariki, Mashariki ya Kati na Oceania yanazingatiwa kama maeneo ambayo maambukizi ya malaria hupatikana kwa asilimia kubwa.
Wataalamu wanaamini kuwa ikiwa ugonjwa huo hautatibiwa mara moja, maambukizi yanaweza kusababisha ugonjwa wa manjano, upungufu wa damu, magonjwa ya figo, kifafa, magonjwa ya akili, kupoteza fahamu na kifo.