Mahakama Nchini Uganda imemuamuru ‘Admin’ wa Group la Whatsapp liitwalo ‘Buyania my Roots’ kumrudisha kwenye group hilo Mwanachama wake aitwae Herbert Baitwababo baada ya Mwanachama huyo kushitaki Mahakamani akidai ‘ameleftishwa’ kwa fitna kwenye group hilo kutokana na kuhoji usimamizi wa pesa.
Baitwababo alisema gharama za kujiunga na group hilo la Whatsapp ni Ush30,000 (Tsh 19,646) ambapo huwa wanatoa michango midogomidogo pale Mtu anapofiwa na Mpendwa wake pia huchanga kwaajili ya matibabu kwa wasio na uwezo pamoja na kuchanga pesa za dharura kama vile matukio ya moto.
Ameendelea kusimulia kwamba alitolewa kwenye group hilo baada ya kuwa na mzozo na mmoja wa Ma-Admin kuhusu usimamizi wa fedha za kikundi hicho na hii ni baada ya kuhoji kuhusu matumizi ya michango iliyokusanywa tangu mwaka 2017 na uhalali wa Kikundi hicho.
Baada ya kushinda kesi hiyo, Herbert Baitwababo aliongea na NTV na kusema maombi yake kwa Mahakama yalikuwa mawili tu ambayo ni yeye kurudishwa kwenye group na pili Mahakama itoe amri ya kudumu ili wasije kumtoa tena.