Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Adolf Ndunguru amewataka Wasimamizi wa Elimu kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha utendaji kazi wao ili kufikia matokeo chanya ya kuboresha elimu yaliyokusudiwa na Serikali katika ngazi zote za elimu.
Ndunguru ameyasema hayo Juni 28, 2023 wakati akifunga mafunzo ya Matumizi ya Njia na Vifaa vya Mtaala wa Elimu ya Awali vilivyoboreshwa kwa Walimu wa Elimu ya Awali yaliyofanyika katika chuo cha Ualimu Mkoani Morogoro.
Amesema kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) kwa mwaka 2022/23 Serikali imetoa jumla ya Shilingi bili. 230 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za msingi 302 zenye vyumba vya madarasa vya mfano vya elimu ya awali, vyumba vya madarasa 2,929, madarasa ya awali ya mfano 368 yanajengwa kwenye shule zilizopo.
“Miundombinu hii itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani, umbali wanaotembea wanafunzi kwenda shule, vikwazo vya usalama wa wanafunzi kufika shule” amesema Ndunguru
Ameongezea kusema, Serikali imeendelea kuajiri walimu ili kuhakikisha kila mwanafunzi anajifunza kwa ufanisi kwa mwaka 2019/20 hadi 2022/23 jumla ya walimu 55,601 waliajiriwa, wakiwemo 2,304 wa elimu ya awali, 29,904 wa elimu ya msingi, na 23,393 wa elimu ya sekondari.
Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuyatumia vyema ikiwemo mada walizofundishwa, mbinu ya kutengeneza zana zinazoendana na mazingira yanayomzunguka mtoto, mbinu shirikishi za kuwezesha ufundishaji kwenye madarasa jumuishi, njia za kushirikisha jamii katika kutoa huduma kwa watoto wa elimu ya awali, miongozo iliyoboreshwa ya ujifunzaji wa wanafunzi wa elimu ya awali na stadi za malezi yenye mwelekeo chanya.
Aidha, amewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha mafunzo ya walimu wanaofundisha elimu ya awali yanaendeshwa kwa ukamilifu na ufanisi kwenye vituo vyote 22 vilivyochaguliwa kama ilivyopangwa.
Ametoa wito kwa Viongozi wa Elimu kuhakikisha walimu wote wanaopatiwa mafunzo wanaporudi vituoni waendelee kupangiwa kufundisha madarasa ya elimu ya awali ili ujuzi wao uendelee kutumika na lengo la kuboresha ujifunzaji wa mwanafunzi wa elimu ya awali lifikiwe.
Kwa upande wa Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimumsingi na Awali TAMISEMI Bi. Susana Nussu amesema, mafunzo yatahusisha washiriki 4,240 wakiwemo wawezeshaji wa kitaifa 110, walimu wanaofundisha elimu ya awali 3000, walimu wakuu 552 na maafisa elimu kata 552.
Amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa afua ya Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi(BOOST).