Mataifa 57 ya Kiislamu Jumapili yamesema kwamba juhudi za pamoja zinahitajika ili kuzuia kudhihakiwa kwa kitabu kitakatifu cha Quran, wakati wakiomba sheria za kimataifa kutumika kusitisha chuki za kidini, kufuatia kuchomwa kwa Quran wakati wa maandamano ya hivi karibuni nchini Sweden.
Taarifa kutoka kwa baraza la ushirikiano wa kiislamu ambalo wengi wa wanachama ni kutoka mataifa yenye wingi wa Waislamu imetolewa baada ya kikao maalum cha kuzungumzia suala hilo kumalizika mjini Jeddah Saudi Arabia, Jumatano wiki iliyopita.
Mwanaume aliyekuwa kwenye maandamano alichoma Quran nje ya msikiti uliopo katikati mwa mji wa Stockholm Jumatano ikiwa siku ya kwanza ya sherehe za Kiislamu za Eid al Adha. Tukio hilo liligadhabisha Uturuki ambayo ni mwanachama wa baraza hilo la kiislamu, na ambayo Sweden, inhitaji uungwaji mkono wake, ili kujiunga na NATO.
Taarifa zaidi zinasema, wanaharakati wa Qur’an wakiwemo wakurugenzi, walimu wa Qur’ani, hii leo Jumatatu watakusanyika mbele ya ubalozi wa Sweden hapa mjini Tehran kwa ajili ya kukemea na kulaani kitendo cha kishenzi cha kuvunjiwa heshima Qur’an tukufu huko Sweden.
Baadhi ya nchi za Kiislamu zikiwemo Pakistan, Uturuki na Yemen pia sambamba na kuendelea kulaani kitendo hicho cha kishetani cha kuchomwa moto Qur’ani Tukufu nchini Sweden, zimetaka kususiwa bidhaa kutoka Sweden.
Siku ya Ijumaa waandamanaji wenye hasira mjini Baghdad wamvamia ubalozi wa Sweden mjini humo kulalamikia kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Sweden na kutaka kutimuliwa mjini humo balozi wa taifa hilo la Ulaya.