Rais wa Marekani Joe Biden amewataka wabunge kuchukua hatua baada ya misururu ya ufyatuaji risasi katika miji mikubwa kuwaua takriban watu 10, jambo linalodhihirisha mapambano yanayoendelea nchini humo dhidi ya utumiaji silaha.
Katika taarifa ya Ikulu ya White House iliyotolewa Jumanne, Biden alitoa wito kwa wabunge wa chama cha Republican kuungana naye katika kuweka “marekebisho ya kawaida”, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku silaha za kushambulia, ukaguzi wa mara kwa mara na kukomesha kinga ya kisheria kwa watengenezaji wa bunduki.
Mwaka jana, mwanamume alifyatua risasi wakati wa gwaride lililoandaliwa karibu na Chicago, Illinois wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya kitaifa ya Julai 4, na kuua watu saba na kujeruhi kadhaa, na kubadilisha “siku hii ya fahari ya uzalendo” katika “msiba”, amekumbusha Joe Biden.
Jumatatu jioni, mtu mwenye bnduki aliwafyatulia risasi watu kadhaa katika mitaa ya Philadelphia (kaskazini mashariki mwa Marekani) na kuua watu watano, wenye umri wa miaka 15 hadi 59 kulingana na polisi, ambayo ilitangaza kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo anashikiliwa na idara za usalama.
Mshambuliaji huyo alikuwa amejihami kwa bunduki aina ya AR-15 na kuwapiga risasi watu hao “kiholela”, kulingana na Kamishna wa Polisi wa Philadelphia Danielle Outlaw.