Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, ametangaza kuwa uchaguzi uliocheleweshwa, utafanyika mwaka ujao kama ilivyopangwa, na kwamba atawania urais.
Salva Kiir, kamanda mkuu wa wapiganaji wa msituni, amekuwa rais pekee wa taifa hilo tangu alipoliongoza kupata uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.
Taifa hilo limeshuhudia migogoro ya mara kwa mara wakati wa uongozi wa Kiir, na linashikiliwa pamoja na serikali dhaifu ya umoja, chini ya uongozi wa Kiir na Makamu wake, Riek Machar.
Kipindi cha mpito kilitarajiwa kuhitimishwa kwa kufanyika uchaguzi, mwezi Februari mwaka huu, lakini serikali hadi sasa imeshindwa kufikia makubaliano muhimu, ikiwa ni pamoja na maafikiano ya kuandaa rasimu ya katiba.
“Ninakaribisha uidhinishaji wa kugombea urais mwaka 2024,” Kiir aliwaambia wafuasi wa chama chake tawala cha Sudan People’s Liberation Movement, akilielezea kama “tukio la kihistoria.”
“Tumejitolea kutekeleza sura za mkataba wa amani uliohuishwa kama ilivyoelezwa, na uchaguzi utafanyika mwaka wa 2024.”
Hakuna mgombea mwingine ambaye ametangaza kugombea, lakini adui wa kihistoria Machar anatarajiwa kugombea.
Mwezi Agosti, viongozi hao wawili waliongeza serikali yao ya mpito kwa miaka miwili zaidi ya muda uliokubaliwa, wakitaja haja ya kushughulikia changamoto zilizokwamisha utekelezaji wa makubaliano ya amani.
Kiir alisema Jumanne kuwa changamoto hizo zitashughulikiwa “kabla ya uchaguzi” uliopangwa kufanyika Desemba mwaka ujao.
Moja ya nchi maskini zaidi duniani licha ya hifadhi kubwa ya mafuta, Sudan Kusini imetumia karibu nusu ya maisha yake kama taifa katika vita.
Takriban watu 400,000 walikufa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano kabla ya Kiir na Machar kutia saini mkataba wa amani mwaka 2018 na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.