Spika wa Bunge la Tanzania ambaye ni Kiongozi wa Msafara wa Tanzania na Spika mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 53 wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF) Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo Julai 5, 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Maspika wa Nchi mbalimbali za Afrika katika ukumbi wa hoteli ya Gran Melia Jijini Arusha ambapo vikao vya Mkutano huo vinaendelea.
Viongozi aliokutana nao ni pamoja na Spika wa Angola Mhe. Pedro Sebastiao, Naibu Spika wa Botswana Mhe. Pono Moatlhodi, Spika wa Zimbabwe Mhe. Jacob Mudenda, Naibu Spika wa DRC Mhe. Sanguma Mossai na Spika wa Lesotho Mhe. Tlohang Sekhamane.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Tulia amewaeleza Viongozi hao kuhusu nia yake ya kugombea nafasi ya Urais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kwa mwaka 2023-2026 huku kauli mbiu yake ikiwa ni “Ufanisi, Uwajibikaji na Uwazi katika IPU”
Viongozi hao wamemshukuru Mhe. Dkt. Tulia kwa namna Tanzania ilivyoshiriki vyema katika maandalizi ya Mkutano huo wa SADC-PF na zaidi wamemtakia kila la kheri katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa IPU unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu katika Mji wa Luanda Nchini Angola.