Mkuu wa mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukuwa hatua Kali dhidi ya watu wanaochepusha maji bila vibali na wanaoharibu vyanzo vya maji kwa kufanya shughuli za uchimbaji wa madini usio rasmi hivyo kupelekea uharibifu katika vyanzo vya maji.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake ya siku moja katika Bwawa la Kuhifadhi Maji la Mabayani na Mtambo wa Kutibu Maji wa Mowe sambamba na kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya maji safi Tanga awamu ya pili.
“Iwe ni marufuku kwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji kuharibu vyanzo hivyo Kwa shughuli za kibinadamu pamoja na kuchepusha maji bila vibali maalum”amesema RC Kindamba.
Aidha alizitaka taasisi za umma ambazo zina madeni makubwa ya ankra za maji kulipa madeni yao ili kusaidia shughuli za uendeshaji kwa TANGA UWASA.
“Ni muhimu tuangalie namna nzuri ya kuhakikisha kuwa Ankara za Maji zinalipwa kwa wakati na madeni yanapungua ili kuiwezesha Tanga UWASA katika utekelezaji wa shughuli zake za kuhakikisha huduma inapatikana kwa wananchi, amesema” RC Kindamba
Pia, Mkurungenzi Mtendaji wa Tanga UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly amesema kuwa mradi wa wa kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya majisafi Tanga awamu ya pili utasaidia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji kutoka lita Mil 30 hadi lita Mil 45 na ameiomba serikali kusaidia katika kuwezesha taasisi za umma kulipia Ankara za maji ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za taasisi.
“Tunaomba serikali itusaidie kuhakikisha baadhi ya taasisi zake zinatulipa malimbikizo ya madeni ambayo mpaka mwezi Juni, 2023 yamefikia takribani sh Bil 9.6 “amesema Mhandisi Hilly.