Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amesema juhudi za kulinda mazingira zinazofanywa na taasisi mbalimbali kuhamasisha nishati safi ya kupikia zinastahili kuungwa mkono.
Pia, ameipongeza Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited (OGTL) kwa kazi nzuri inayoifanya kuiwezesha jamii kupata gesi safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi na majiko yake kwa wananchi, hivyo kutekeleza mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Dk. Mpango alisema hayo kwa wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, mkoani Kigoma katika hafla ya kukabidhiwa kwa vifaa mbalimbali kwa wanawake wajawazito ikiwemo mitungi ya gesi 300 iliyokabidhiwa kwa wajawazito 214 na watumishi wa afya ngazi ya jamii 86 kutoka wilaya hiyo.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Oryx Gas Kanda ya Kaskazini, Alex John, amesema kampuni hiyo ikiwa kinara wa soko katika usambazaji wa gesi ya kupikia nyumbani (LPG) nchini, inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali za kuhimiza matumizi ya nishati hiyo.
Ameongeza gesi safi ya LPG ni suluhisho la kutokomeza matumizi ya kuni na mkaa, hivyo kuboresha afya ya jamii, ustawi na utunzaji wa mazingira, pia ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kama mkakati wa kulinda mazingira.