Kampuni mama ya Tembo Nickel Lifezone Metals, imeanza kuuza hisa zake katika soko la hisa la New York nchini Marekani.
Tembo Nickel ni kampuni ya uchimbaji wa madini ya Nickel iliyo Ngara mkoani Kagera ambapo Serikali ya Tanzania ina hisa asilimia 16.
Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Dr Elsie Kanza, akizungumza baada ya tukio la kampuni hiyo kuanza kuuza hisa, alisema ni moja ya ishara ya kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi.
Naye Mwenyekiti wa Tembo Nickel Lifezone Metals, Keith Liddell, amesema Lengo la Kampuni yake ni kudumisha nishati salama kwa ulimwengu kwa kuzalisha Nickel kwa njia salama kwa mazingira na kuleta majibu sahihi kwa uchafuzi wa hali ya hewa duniani.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Tembo Nickel, Benedict Busunzu, amesema ni furaha wawekezaji wa kimataifa wataanza kuwekeza kwenye kampuni itakayochimba na kuzalisha metali safi nchini Tanzania kuanzia hatua ya mwanzo hadi mwisho.
“Wawekezaji wa kimataifa sasa wanaweza kuwekeza kwenye kampuni ya madini ambayo inaanza kwenye uchimbaji hapa nchini hadi kwenye kupata bidhaa ya mwisho.”
Busunzu ameishukuru Serikali ya Tanzania ya kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.
Kiwanda cha kuchenjua madini ya Nickel kinatarajiwa kuwa Kahama mkoani Shinyanga.