Wakazi 2,884 katika Kata 206 za Mkoa wa Tabora watanufaika na miradi ya kiuchumi ya Tsh. milioni 81 watakayoibuni kupitia kamati za utekelezaji za Kata hizo hii ikiwa ni moja ya mbinu aliyokuja nayo Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Tabora (CCM), Jacqueline Kainja katika kuwainua Wananchi kiuchumi ambapo amewataka Wabuni miradi kisha atawapa pesa kutoka mfukoni mwake watekeleze miradi hiyo.
Akiongea wakati akikabidhi fedha hizo kwa Wajumbe wa Kamati za Utekelezaji za Kata za Mkoa huo kwenye hafla ya uzinduzi wa miradi hiyo kupitia Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Tabora, Kainja amesema fedha hizo zitasaidia kuwapa nguvu katika miradi ya kiuchumi watakayoibuni kwenye Kata zao.
“Tunataka wanufaika hao wawe chachu ya kunufaika ili watakaponufaika basi inufaishe jamii yote inayowazunguka kwenye kata zao na mimi naahidi nitasaidia hata makundi ya Vijana wakiwemo bodaboda lakini mkazo utakuwa zaidi kwa wanawake”
“Mwaka 2021 nilitoa ahadi kwamba nitawapa Wananchi pesa wafanye miradi mbalimbali kutokana na mazingira, gharama ya kukamilisha mradi wote ni Tsh. Milioni 81, Katibu Tawala wa Mkoa amezindua rasmi ugawaji wa fedha hizo na sasa nimeanza kuzunguka Kata mbalimbali za Mkoa wa Tabora kugawa fedha hizo”