Nahodha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ghana Asamoah Gyan amewaasa wadau wa soka hasa toka Serikalini kuunga mkono juhudi za wanasoka wa zamani katika kuendeleza mchezo huu pendwa katika Mataifa mbalimbali Afrika.
Gyan alizungumza hayo kwenye Kongamano maalum lililoandaliwa Rabat Morocco agenda Kuu ikiwa kuboresha uhusiano kati ya Morocco na Mataifa ya Kusini Morocco-South Cooperation.
Asamoah akiwa miongoni mwa Wachezaji wakubwa wa zamani walio na hadhi za Malejendari au magwiji kama Kalusha Bwalya, El Hadji Diouf, Emanuel Adebayor na Alexander Song alisema kuwa kila mmoja anauliza wachezaji wa zamani nini watafanya baaada ya kustaafu kuendeleza soka lakini hakuna aliye tayari kuchangia chochote au kuunga mkono kile wanachoweza kufanya Wachezaji hawa.
Kwa sasa Asamoah yuko kwenye hatua za kufungua kituo chake cha kuendeleza vipaji huku akiwa tayari anawakilisha baadhi ya wachezaji ambao wanacheza kwa sasa.
Gyan atakumbukwa kama mtu anayeongoza kwa mabao kwenye Kombe la Dunia toka Ghana lakini wengi watakumbuka penati aliyokosa kwenye mchezo dhidi ya Uruguay kwenye robo fainali ya FIFA World Cup 2010 ambapo mkwaju huo ungeipeleka Ghana nusu fainali endapo wangeshinda mchezo huo.