Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa Afrika yaliyofanyika Jijini Arusha leo July 11,2023 ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni kwamba katika jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa Serikali ya Tanzania kuanzia mwaka wa fedha 20219/2020 hadi mwaka wa fedha 2021/2022 imefanikiwa kuokoa na kudhibiti matumizi ya fedha yasiyostahili ya zaidi ya Tsh bilioni 139.
Rais Samia amenukuliwa akisema “Tumeongeza uwazi katika matumizi ya fedha za umma na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, kwa kuanzia mwaka wa fedha 20219/2020 hadi mwaka wa fedha 2021/2022 tumefanikiwa kuokoa na kudhibiti matumizi ya fedha yasiyostahili ya zaidi ya Tsh bilioni 139 ambacho ni kiasi kikubwa kidogo kwa fedha za umma”
“Pesa hizo ukinipa Mimi nakuambia nazipeleka kununua vifaa tiba ili vituo vyangu vyote vya afya na zahanati nilizojenga viwe na vifaa tiba”
Maadhimisho hayo ya siku tatu yanafanywa kwa kuendeshwa kongamano la wadau ambao watajadili uzoefu wa Afrika katika kupambana na rushwa.
Aidha, katika maadhimisho hayo Bodi ya Umoja wa Afrika Mapambano ya Rushwa watatoa mrejesho na pia Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) na Takukuru nao watazungumzia uzoefu wao.
Pia elimu kuhusu maadili, utawala bora, uhujumu uchumi, jinsi ya kupambana na rushwa, madhara ya dawa za kulevya, na mabanda ya utalii yatakuwepo.