Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amemtaka Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki Mhe.Idd Seif Bakari kuendeleza uhusiano uliopo , kudumisha diplomasia ya kiuchumi , kusaidia kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji pamoja na biashara zipatikanazo katika nchi ya Uturuki.
Ameyasema hayo leo alipokutana na Balozi Idd Seif Bakari aliyefika Ikulu Zanzibar kumuaga kuelekea katika kituo chake cha uwakilishi nchini Uturuki baada ya uteuzi wake hivi karibuni.
Aidha, Rais Dk Mwinyi amegusia mambo matatu katika kufungua fursa za uwekezaji na biashara kati ya Zanzibar na Uturuki ikiwemo kupata wawekezaji katika viwanda kwa maendeleo waliyopiga kupitia sekta hiyo kuja kuwekeza nchini, eneo la pili kuzitangaza fursa zilizopo katika sekta ya utalii wa fukwe za bahari na urithi pia kupitia kuwepo kwa usafiri wa ndege ya shirika la Uturuki linalofanya safari zake za moja kwa moja hapa nchini kutangaza vivutio vinavyopatikana nchini, eneo la tatu kujifunza na kutafuta fursa za uwekezaji zitokanazo na sekta ya miundombinu ikiwemo bandari, barabara, na viwanja vya ndege.
Balozi Idd Seif Bakari aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Aprili 05 Mwaka huu, kabla ya uteuzi huo alikuwa Konseli Mkuu, Dubai.