Uingereza na Ukraine zimekubaliana kwamba mipango mipya ya usalama ambayo itatangazwa na washirika wa kimataifa haitakuwa mbadala wa uanachama wa Ukraine wa NATO, kulingana na ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak.
“Waziri Mkuu na Rais walikubaliana juu ya umuhimu wa mipango ya usalama kutangazwa na G7 mchana huu,” ofisi ya Sunak ilisema, baada ya kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy katika mkutano wa kilele wa NATO nchini Lithuania.
“Wote wawili walikubaliana kwamba mipango haitakuwa mbadala wa uanachama wa NATO na wanatarajia kujenga mfumo mpya wa usalama haraka iwezekanavyo.”
Dmytro Kuleba, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ukraine, amesema kuwa Ukraine itaridhika na mtindo wowote wa usalama na ulinzi mradi tu haijawekwa kama mbadala wa uanachama wake wa NATO.
Nukuu kutoka kwa Kuleba: “Hatuhitaji Mkataba mwingine wa Budapest, tuliposalimisha silaha za nyuklia kwa kubadilishana na ahadi tupu. Hatutaacha uanachama wa NATO. Kwa sababu kila mtu anaelewa – na washirika wetu wote wanaelewa – kwamba uanachama wa Ukraine katika Umoja huo ni hakikisho thabiti zaidi kwamba hakutakuwa na vita vingine huko Urope.
Dhamana zingine zote za usalama ni sawa. Lakini hakuna mbadala wa uanachama wa NATO huu ni msimamo thabiti wa rais [wa Ukraine], na utapitishwa kupitia maamuzi yanayochukuliwa.”
Kuleba alitoa kauli hii baada ya kuulizwa iwapo Ukraine itakubali dhamana za usalama zinazotolewa kwa mfano zile zilizopewa Israel.
Israel ni mshirika thabiti zaidi wa Marekani katika Mashariki ya Kati; Mikataba ya miaka 10 inaeleza ahadi za Marekani kwa nchi hiyo, chini ya mkataba wa hivi punde zaidi ambao Marekani itasambaza msaada wa dola bilioni 38 mwaka 2019-2028.
Kuleba aliongeza kuwa Ukraine inapaswa kutekeleza maamuzi ya mkutano wa Vilnius ili kuharakisha ushirikiano wake wa Euro-Atlantic: “Mpango A ni uanachama wa NATO wa Ukraine. Swali ni je, tunafikaje huko haraka iwezekanavyo?”