Rais wa Manabii na Mitume Tanzania Nabii Joshua amewataka watanzania kua watulivu wakati serikali inaendelea na mchakato wa mkataba wa Bandari na kampuni ya DP World .
Nabii Joshua ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Morogoro ambapo amesema hapingi watu wanavyotoa maoni kuhusu mchakato wa mkataba lakini namna ya uwasilishaji maoni baadhi ya watu umekua tofauti kwa matumizi ya Lugha kwa viongozi Serikalini jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Anasema kama kiongozi wa dini anawajibu wa kuwakumbusha watu suala la utuzaji amani hivyo anaomba mjadala uwe mzuri kuzingatia matumizi ya lugha kwa viongozi ili waendelee kuleta majibu yenye ufanisi kwa Wananchi wao.
Nabii Joshua anasema tayari viongozi mbalimbali wa serikali wameshatolewa ufafanuzi baadhi ya mambo ambayo yamekua mjadala kwa Wananchi hivyo njia rahisi ya uwasilishaji maoni ni kutumia Mamlaka husika ili waweze kuyafanyia kazi badala ya kutumia mitandao kutoa lugha zisizo za stara.
Aidha ameiomba Serikali kutopuuza maoni ya Wananchi badala yake wasikilizwe na yafanyiwe kazi ili kiu na matamanio yao yaweze kupata majibu yaliyosahihi kwa maslahi mapana ya Taifa kwa ujumla.
Ikumbukwe kua mjadala mkubwa wa Mkataba wa Bandari kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ni ukomo wa mkataba na maslahi kwa taifa huku Wananchi wakiomba kupata ufafanuzi wa vifungu vya mkataba huo.