Taasisi ya uhifadhi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) kwa kushirikiana na Kampuni ya Utalii ya Mwiba Holdings LTD wamezindua mradi wa kutoa chakula cha bure cha mchana kwa wanafunzi 856 wa shule ya Msingi Makao,wilayani Meatu mkoa wa Simiyu..
Mradi huo umezinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura ambapo kampuni hizo zitakiwa zikitumika kiasi cha shilingi milioni 20.5 Kila mwezi kwa ajili ya kutoa chakula hicho cha mchana pamoja na kujenga jiko la kisasa kwa ajili ya shule hiyo ambalo limegharimu kiasi Cha shilingi milioni 28.1. na mradi wa uvunaji Maji ya mvua uliogharimu shilingi milioni 30.8 .
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo,Mkuu huyo wa wilaya alipongeza Taasisi ya Friedkin na Mwiba Holdings kwa kutoa msaada huo mkubwa kwa wilaya ya Meatu ambao unaendana na Maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora huku akisema mradi huo utasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi ,kuondoa utoro lakini pia kuwapa Utulivu wanafunzi wakiwa darasani.
Wakizungumzia mradi huo,Meneja wa miradi ya Maendeleo ya Jamii wa Friedkin Tanzania, Aurelia Mtui na Meneja miradi Maendeleo ya Jamii wa Friedkin Wilayani Meatu, Sylvester Bwasama wamesema mradi huo ni sehemu ya miradi inayofanywa kwenye Jamii zinazozunguka maeneo ya vijiji zaidi ya 25 katika wilaya hiyo waliowekeza shughuli za uhifadhi na Utalii.
Bwasama amesema licha ya mradi huo pia wanamradi wa ukamilishaji nyumba ya walimu na madarasa mawili katika shule ya msingi Mwajimoso iliyopo Kijiji cha Mwambagimu,mfumo wa uvunaji Maji ya mvua shule ya sekondari Makao,tunawezesha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na vijana kuelewa umuhimu wa Utalii na uhifadhi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Meatu, Anthony Philipo alisema miradi hiyo iliyozinduliwa inatoka na ushirikiano mzuri uliopo sasa baina ya mwekezaji katika eneo la Ranchi ya Mwiba na Makao WMA.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Makao John Saganda alipongeza mradi huo ikiwepo kununua vifaa kama masufuria, sahani, vijiko na vifaa vingine ambavyo vimegharimu shilingi milioni 3.7.
Saganda alisema pia wao kama Jamii inayozunguka maeneo ambayo Kampuni ya Mwiba inaendesha shughuli za Utalii na uhifadhi watakuwa mabalozi wazuri kuhakikisha wanyama wanalindwa na mazingira hayaharibiwi.