Bodi ya Korosho Tanzania katika kusimamia maendeleo ya Tasnia imeweka malengo makuu matatu ambayo ni: Kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi kufikia tani 1,000,000 ifikapo 2030 Kubangua asilimia 60 ya korosho hizo na Kuwa na masoko ya uhakika na endelevu ya korosho na bidhaa zake ifikapo 2030 ili kufikia agenda 10/30. Agenda 10/30 inaelekeza sekta ya kilimo kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa na kuingiza fedha za kigeni kwa wingi.
Kwa mujbu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2022, zao la korosho liliongoza kwa kuliingizia Taifa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 226.9 ikilinganishwa na mazao mengine ya tumbaku (USD 178.5M); kahawa (USD 161.2M); pamba (USD 103.4M); karafuu (USD 42.18M); chai (USD 30.0M) na mkonge (USD 24.3M).
Aidha ni wazi kuwa fursa zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho zikitumika kwa ufanisi Taifa linaweza kujipatia fedha nyingi zaidi za kigeni.
Mkutano huu unakusudia kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho kuanzia shambani ambapo tunategemea kupata uwekezaji wa kwenye 2 mashamba makubwa, Ubanguaji ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika korosho na bidhaa zake na kuimarika kwa masoko kwa kufungua masoko ya korosho na bidhaa zake ndani na nje ya nchi.
Kwa upekee Mkutano huu utatumika kuhamasisha matumizi ya korosho na bidhaa zake ndani ya nchi kama vile mafuta ya ganda la korosho (Cashewnut Shell Liquid – CNSL), sharubati (juice), maziwa ya korosho (cashew milk), mvinyo (wine), nyama ya mabibo (cashew apple meat) na pombe kali.
Aidha bidhaa nyingine kama ethanol zinaweza kutumika kwenye maabara za hospitali na shule zetu na hivyo kupanua wigo wa soko la korosho. 3.0 WASHIRIKI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA KOROSHO WA MWAKA
Mkutano wa Kimataifa wa Korosho wa Mwaka 2023 unakusudiwa kuhudhuriwa na washiriki 500 kutoka nchi zote Duniani zikiwemo nchi 33 zinazolima korosho. Nchi hizo ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania. Aidha, mkutano huo utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika. Mkutano unakusudia kuwa na washiriki wote walioko kwenye mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Korosho kama vile wakulima, wabanguaji, wasindikaji, wakaangaji, wasafirishaji, Vyama vya Ushirika, Wasambazaji wa pembejeo, waendesha ghala, watafiti, wazalishaji wa mitambo na vipuli, wasimamizi wa Tasnia, walaji au watumiaji wa bidhaa za korosho, Taasisi za fedha, watunga sera, wawekezaji, wabia wa maendeleo na wadau wengine wengi.