Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema kupitia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025 ndani ya kipindi cha miaka miwili na nusu tayari miradi mingi ya maendeleo imekamilika na sasa ni kuendelea kuongeza juhudi zaidi kwenye kuimarisha sekta ya miundombinu ikiwemo barabara zitakazotumika zaidi ya miaka 60 mbele, ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa Pemba, utakaojumuisha barabara ya kilomita 2.5 pamoja na jengo jipya la abiria ili kukifungua kisiwa kwa uwekezaji, utalii na kutoa ajira mpya kwa wananchi.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika mkutano wake na Mabalozi, Wajumbe Halmashauri za CCM Majimbo, Wilaya na Mkoa katika ukumbi wa Umoja ni Nguvu uliopo Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba kwa ziara ya kichama na kukagua mali za CCM.
Aidha, Makamu Mwenyekiti Dk.Mwinyi ameahidi ujenzi wa kumbi za mikutano za kisasa kwa Unguja na Pemba zenye uwezo wa kubeba mikutano mikuu ya Chama kitaifa.
Vilevile, Makamu Mwenyekiti Dk.Mwinyi amemuagiza Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Dimwa kuanza kutoa vitambulisho vya mabalozi kwa ajili ya utaratibu wa malipo ya posho la kujikimu kwa mwezi kwa Mabalozi hao.