EWURA imepokea taarifa ya uwepo wa baadhi ya Kampuni za Mafuta KUHODHI mafuta kwa ajili ya maslahi binafsi ya kibiashara ikiwemo kusubiri mabadiliko ya bei.
Aidha, kampuni nyingine zinasemekana kupakia mafuta kutoka kwenye maghala pasipo kuyauza na nyingine kukataa kuza mafuta kwa wamiliki wa vituo wasio kuwa na ubia au mikataba nao.
Kutokana na hayo, EWURA imepata taarifa ya kuchelewa kufikishwa kwa mafuta katika baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa nchi na miji.
EWURA inapenda kuwajulisha wananchi wote kuwa Nchi ina mafuta ya kutosha katika maghala ya kuhifadhia mafuta na wakati huo huo meli zenye shehena ya mafuta kutoka nje ya Nchi zinaendelea kuingia na kushusha mafuta kama kawaida chini ya uratibu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
Mpaka tarehe 14 Julai 2023 mafuta yote yaliyokuwepo chini ni lita 169,853,692 za mafuta ya petroli, lita 209,641,670 za diezeli na lita 34,588,002 za mafuta ya ndege yanayotoshelea mahitaji. Kutokana na taarifa hizo, EWURA inatoa ONYO kwa kampuni za mafuta zinazohodhi mafuta na kuzitaka kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni zinazosimamia biashara ya mafuta ya petroli nchini na masharti ya leseni zao za biashara.
EWURA inapenda kuwataarifu wananchi kuwa inaendelea kufanya ukaguzi wa kina kwenye maghala na vituo vya mafuta na kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaothibitika kukiuka sheria, kanuni za masharti ya leseni zao, ikiwemo kuwanyang’anya leseni ya biashara kwa mujibu wa Kanuni Namba 6 ya Kanuni Ndogo za Ukokotoaji wa Bei za Mafuta GN. 57 ya mwaka 2022.