Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limemkamata dereva wa bajaji katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi, Ayubu Mng’osi (30) kwa tuhuma za kubaka na shambulio la aibu kwa watoto wawili wenye umri wa miaka 7 na 9 ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne 18, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya amesema kuwa katika tukio la kwanza, mtuhumiwa huyo anadaiwa kumwingilia kimwili mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya Msingi Ichenjezya (Jina limehifadhiwa).
“Mbinu aliyotumia mtuhumiwa ni kumlaghai mtoto na kuingia naye ndani ya nyumba anayoishi kisha kumuingilia kimwili” amesema
Aidha Kamanda Theopista amesema kuwa mtuhumiwa huyo pia anadaiwa kumfanyia shambulio la aibu la kumshika na kumchezea sehemu za siri mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya Ichenjezya Wilayani Mbozi (naye jina limehifadhiwa).
“Julai 14 mwaka huu maeneo ya Mianzini Kata ya Ichenjezya myoa taarifa aligundua kushikwa, kuchezewa sehemu za siri maeneo ya makalioni kwa mjukuu wake mwenye umri wa miaka 7 mwanafunzi wa darasa la pili na Ayubu Mng’osi” ameeleza
Kamanda huyo ameeleza kuwa mbinu alizotumia mtuhumiwa huyo ni kuwaingiza watoto hao ndani kwake kwa siku moja kuwafanyia vitendo hivyo vya kinyama.
“Mtuhumiwa amekamatwa na upelelezi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo kwa ajili ya kufikishwa mahakamani” ameeleza kamanda huyo.