Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar ni nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa Mwani katika bara la Afrika uzalishaji umeongezeka zaidi kwa tani 12,594 kwa mwaka 2021/22 licha ya kuwa na ushindani na wazalishaji wakubwa duniani kama China, Ufilipino, Indonesia na wengine.
Ameyasema hayo leo akifungua Maadhimisho ya nane ya siku ya Mwani Zanzibar yaliyofanyika ukumbi wa Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha , Rais Dk.Mwinyi amesema mafanikio yote yanatokana na utekelezaji wa sera na mikakati ya uchumi wa buluu ambapo Serikali imeweza kuunda sera mpya ya uchumi wa buluu pamoja na mikakati ya uzalishaji wa mazao ya baharini ukiwemo Mwani.
Vilevile, Serikali kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imewekeza fedha nyingi sana katika kuwasaidia wakulima na wajasiriamali wa sekta ya mwani wapatao 5,000 Unguja na Pemba kwa kuwapatia boti maalumu za kuwawezesha kwenda katika maji ya kina kirefu zaidi kwa ajili ya ulimaji wa mbegu bora za mwani na kujiepusha na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi alieleza Serikali ya Korea imeleta mradi mpya wa mwani wenye thamani ya zaidi ya bilioni 10 utakaoanza mwezi Agosti mwaka huu kwa kuwaendeleza zaidi Wanawake katika uwezeshaji , ubunifu wa kuwapatia nyenzo za usarifu wa zao la mwani.
Rais Dk Mwinyi ametoa shukrani maalumu kwa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) kwa kuwa karibu na wakulima wa mwani na kujitolea kwao kuhakikisha shabaha za kumkomboa Mwanamke kiuchumi kupitia Uchumi wa Buluu inafanikiwa.