Ikulu ya White House inasema haiungi mkono mashambulizi ndani ya Urusi baada ya kuulizwa kuhusu ndege mbili zisizo na rubani kutoka Ukraine ambazo ziliharibu majengo mjini Moscow mapema Jumatatu.
“Kama jambo la jumla hatuungi mkono mashambulizi ndani ya Urusi,” msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano na waandishi wa habari.
Urusi ilizungumza kuhusu kuchukua hatua kali za kulipiza kisasi dhidi ya Ukraine baada ya mashambulizi hayo mawili ya ndege zisizo na rubani, likiwemo lile lililo karibu na makao makuu ya wizara ya ulinzi, katika kile ilichokiita kitendo cha ugaidi.
Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulio hilo mjini Moscow — la hadhi ya juu zaidi ya aina yake tangu ndege zisizo na rubani mbili kufika Kremlin mwezi Mei.
Ndege moja isiyo na rubani ilipiga karibu na makao makuu ya ulinzi ya Urusi katika pigo la ishara ambalo lilisisitiza kufikiwa kwa ndege kama hizo, na afisa mkuu wa Ukrain alisema kutakuwa na mashambulio zaidi.
Wakati huo huo, Kyiv siku ya Jumatatu ilisema shambulio la ndege isiyo na rubani ya Urusi liliharibu maghala ya nafaka ya Ukraine kwenye Mto Danube na kuwajeruhi watu saba.
Kremlin ilisema itaendelea na kile inachoita “operesheni yake maalum ya kijeshi” nchini Ukraine. Kyiv na sehemu kubwa ya Magharibi wanasema ni vita vya kikatili vya ushindi.