Waziri wa Usafi wa Mazingira na Maji Cecilia Abena Dapaah, ambaye alijiuzulu mwishoni mwa juma “amekamatwa kwa tuhuma za ufisadi kuhusu kiasi kikubwa cha pesa… zinazodaiwa kuibwa nyumbani kwake,” Mwanasheria Mkuu Kissi Agyebeng alisema Jumatatu.
Bi Dapaah amekana kufanya makosa yoyote, lakini kesi hiyo imeukasirisha upinzani, ambao wanashangaa kwa nini waziri aliweka pesa nyingi katika makazi ya familia yake. Kulingana na nyaraka za mahakama, wafanyakazi wawili wa nyumbani wanadaiwa kuiba dola milioni 1, euro 300,000 na mamilioni ya cedi za Ghana kutoka chumba cha kulala cha waziri mwaka jana.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Bi Dapaah aliwasilisha ombi la kujiuzulu huku akikana kwamba pesa nyingi kama hizo ziliibiwa. “Ingawa ninaweza kusema kwa dhati kwamba nambari hizi haziwakilishi kwa usahihi kile ambacho mimi na mume wangu tuliripoti kwa polisi, ninafahamu kabisa umuhimu wa hadithi kama hizo kwa mtu wa nafasi yangu,” aliandika. “Kwa hiyo najiuzulu kwa sababu sitaki jambo hili liwe wasiwasi kwa serikali na kuwa kikwazo kwa kazi yake.”
Kashfa hii inakuja wakati nchi hiyo ikipitia mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, jambo ambalo limeifanya serikali kuomba mkopo wa dola bilioni tatu kutoka kwa IMF.