Thomas Tuchel alimsifu mchezaji mpya aliyesajiliwa na Bayern Munich Kim Min-jae kama usajili muhimu sana siku ya Jumanne lakini akasema kuna uwezekano atasalia nje mechi ya kwanza ya mabingwa hao wa Ujerumani katika ziara ya maandalizi ya msimu mpya nchini Japan.
Raia huyo wa Korea Kusini alijiunga na Bayern wiki iliyopita, baada ya kushinda Serie A msimu uliopita akiwa na Napoli.
“Alicheza msimu mzuri sana nchini Italia na katika Ligi ya Mabingwa,” kocha wake mpya aliwaambia waandishi wa habari mjini Tokyo.
“Alikuwa wa kutegemewa sana, ulinzi mkali sana, uchezaji mzuri wa kujijenga. Mkamilifu sana na tunatumai anaweza kutulia haraka sana na kuwa beki ambaye alikuwa zamani.”
Kim amecheza mechi 49 za kimataifa na alicheza katika nchi yake ya Korea Kusini na Uchina kabla ya kusajiliwa na Fenerbahce ya Uturuki na kisha kuhamia Napoli msimu uliopita wa joto.
Tuchel alisema “maendeleo ya beki huyo wa kati yanajieleza yenyewe”.
“Alifanya hivyo hatua kwa hatua na kwa kila mabadiliko ya klabu alichukua kiwango kipya cha mchezo wake,” Tuchel alisema.