Historia imeandikwa kwenye Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake huku Nouhaila Benzina, mwanasoka wa kwanza aliyevalia Hijabu alipoingia uwanjani kuiwakilisha timu ya Taifa ya Morocco.
Hiyo pia ni mara ya kwanza kwa timu ya wanawake kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kushiriki mashindano hayo. Ingawa Morocco ilishindwa na Ujerumani kwa mabao 6-0 Jumatatu kwenye Uwanja wa Melbourne, lakini wapenzi wa soka kutoka mataifa ya Kiarabu wana matumaini kuwa timu hiyo itarejea kwa nguvu katika maechi zake zinazokuja.
Benzina, mchezaji kandanda mwenye umri wa miaka 25, ambaye pia anachezea Klabu ya Soka ya Jeshi la Kifalme la Morocco (FAR), alijiunga na timu ya taifa mwaka 2018. Kabla ya hapo, beki huyo wa Morocco alionyesha kipawa chake alipokuwa akiichezea timu ya wasichana walio na umri wa chini ya miaka 20 ya Morocco mwaka 2017.
Uwepo wake uwanjani ni muhimu hasa kutokana na kuibuliwa mijadala inayohusu ujumuishaji wa Hijabu katika michezo. Nouhaila anasimama kama nembo ya uthabiti na azma ya wanawake wa Kiislamu ambao wamepigana kwa miaka mingi kuondoa marufuku ya chuki dhidi ya Uislamu iliyowekwa na FIFA kuhusu vazi la stara la Hijabu.
Marufuku hiyo, ambayo iliwekwa mwaka 2014, imekuwa na athari mbaya kwa wanawake wanaotaka kuwa wanamichezo waliovalia Hijabu.
Mojawapo ya mifano ya mapema zaidi ya chuki dhidi ya vazi la Hijabu ni ile ya Asma Mansour mnamo 2007, ambaye alizuiwa kucheza katika mashindano huko Quebec nchini Canada kutokana na kuvalia kwake Hijabu. Ni matukio kama hayo ndiyo yaliibua vuguvugu la kutetea haki ya kuvaa hijabu wakati wa michezo ya soka.
Mnamo 2014, FIFA hatimaye iliondoa marufuku hiyo katika uwanja huo.