Rais Putin alitia saini sheria hiyio ya kupiga marufuku upasuaji wa kubadili jinsia siku ya Jumatatu. Sheria hiyo inayolenga kusimamia na kuweka udhibiti mkali wa kile ambacho wabunge wa Russia amekieleza kama “tasnia ya watu wanaobadili jinsia,” inapiga marufuku mabadiliko ya jinsia isipokuwa kwa sababu za kiafya na kimatibabu.
Matibabu na upasuaji unaohusishwa na kubadilisha jinsia sasa utaruhusiwa tu katika hali zinazohitajia matibabu ya ulemavu wa viungo vya uzazi kwa watoto. Ni kliniki zilizo na leseni kutoka Wizara ya Afya ya Russia tu ndizo sasa zitaweza kufanya maamuzi juu ya matibabu kama hayo na kutoa vyeti vinavyohitajika katika uwanja huo.
Raia hawataruhusiwa tena kubadilisha jinsia zao kwa uhuru kwenye vitambulisho na hati nyingine za utambulisho kama ilivyokuwa imezeeleka.
Wale waliofanya hivyo wanaweza kuzuiwa kuasili watoto chini ya sheria mpya. Wanandoa pia wataweza kubatilisha ndoa zao ikiwa mmoja wao atabadilisha jinsia yake.
Kwa mujibu Evgenia Kotova, Naibu Waziri wa Afya wa Russia, zaidi ya Warusi 2,000 walibadilisha jinsia zao kisheria nchini humo kati ya 2018 na 2022, wakati jambo hilo lilikuwa linaruhusiwa.
Spika wa Bunge la Russia, Duma, Vyacheslav Volodin ameshambulia vikali kile amekiita ‘sekta ya wabadilishaji jinsia ya Magharibi’ na kutetea hoja iliyopelekea kubuniwa sheria hiyo mpya ya jinsia nchini humo. Amesema idadi ya upasuaji wa kubadili jinsia nchini Marekani imeongezeka mara 50 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, na kuongeza kuwa karibu asilimia 1.4 ya vijana wa Marekani wenye umri wa kati ya miaka 13 na 17 walijitambulisha kuwa watu waliobadili jinsia mwaka 2022.