Imebainika kuwa Mjini Songea kuna kesi nyingi za malalamiko ya Wanawake kupigwa na Wanaume zao na kufanyiwa ukatili wa kiuchumi ambapo wakati wa mavuno ya mazao Wanaume huwafukuza Wake zao majumbani.
Askari Polisi kutoka dawati la jinsia na Watoto Polisi Wilaya ya Songea, Sajenti Mwanaisha Ndauka amesema kesi hizo ni nyingi na wanaendelea kukabiliana nazo, hayo ameyasema wakati wa muendelezo wa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) kwa Mkoa wa Ruvuma ambapo Wataalamu wanaendelea kutembelea maeneo mbalimbali kutoa elimu na leo walikuwa Mtaa wa Makambi Kata ya Ndirima Litembo.
Eva Zambo ni Mwananchi ambaye anasimulia namna alivyoachana na Mumewe aliyezaa nae Watoto wanne bila kupewa talaka wala kupata mirathi na anakiri Kampeni ya Mama Samia Legal Aid itamsaidia.
Itakumbukwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango July 22, 2023 alizindua Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) kwa Mkoa wa Ruvuma, katika Uwanja wa Majimaji uliopo Songea Mkoani humo ikiwa ni mkakati unaotekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wenye lengo la kuongeza uelewa wa sheria na haki za binadamu kwa Wananchi wote hususani Wanawake, Watoto na makundi maalum, na baada ya uzinduzi tayari Timu ya Kampeni hiyo inaendelea kuzunguka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma kutoa elimu: