Zaidi ya watoto 40,000 ambao wamekimbia mapigano nchini Sudan hadi Sudan Kusini tangu Aprili sasa hawawezi kwenda shule, Umoja wa Mataifa unasema.
Kwa mujibu wa ofisi ya umoja wa mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu (Ocha), zaidi ya watu 183,000 hadi sasa wamevuka mpaka tangu mzozo kati ya makundi hasimu ya kijeshi ya Sudan kuanza.
Idadi hii inatarajiwa kuongezeka huku vita vikiendelea na majaribio ya kupata mwafaka wa kusitisha mapigano yakiendelea.
Wale wanaowasili katika Jimbo la Unity, kwenye mpaka na Sudan, walikuwa na majeraha na waliripoti matukio ya uporaji na unyanyasaji na makundi yenye silaha wakati wa safari yao, Ocha ilisema.
Wengi wao ni raia wa Sudan Kusini ambao walikuwa wamehamia Sudan katika muongo mmoja uliopita ili kuepuka machafuko nyumbani ambapo sasa wamelazimika kutoroka tena.