Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuendeleza mazungumzo ya kidini, ambayo pamoja na mambo mengine, inachukizwa vikali na vitendo vyovyote vinavyolengwa dhidi ya vitabu vitakatifu na kutambua matukio hayo kuwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa, msemaji wa rais wa baraza hilo amesema.
Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinishwa baada ya Qur’ani Tukufu kuvunjiwa heshima katika nchi za Sweden na Denmark, suala ambalo limeibua hasira na na malalamiko makali ya mataifa ya Kiislamu kote duniani.
Azimio lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalaani vikali vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watu kwa misingi ya dini au imani zao, na kitendo chochote kinachopiga vita alama za dini, vitabu vitakatifu, nyumba, biashara, mali, shule, vituo vya kitamaduni au maeneo ya ibada. Azimio la Baraza Kuu la UN pia limelaani shambulio lolote dhidi ya maeneo ya kidini, maeneo ya ibada na maeneo matakatifu ya kidini na kutangaza vitendo hivyo kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Tarehe 12 mwezi huu wa Julai pia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio lililopendekezwa na nchi za Kiislamu la kulaani kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu na kumtaka Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kufanya uchunguzi kuhusu jambo hilo pamoja na kutoa ripoti kuhusu uchunguzi huo.
Azimio hilo pia linaitaka Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu na mifumo mingine ya Baraza la Haki za Binadamu kutoa mapendekezo yanayohitajika kwa nchi zote ili kuziwezesha kurekebisha mapungufu ya kisheria yanayochochea kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini.