Balozi wa Tanzania nchini Korea ya kusini Togolani Mavura ametembelea kiwanda cha kampuni ya Hyundai Rotem na kukagua maendeleo ya utengenezaji wa seti 10 za treni za kisasa na vichwa 17 vya treni vya umeme mjini Changwon, Korea ya kusini.
Akiwa katika karakana inayotengeneza seti za treni za kisasa (EMU) Balozi Mavura ameeleza kuridhishwa na kazi iliyofanyika mpaka sasa na kuwatoa hofu Watanzania juu ya maendeleo ya utengenezaji wa vifaa hivyo vitakavyotumika katika reli ya kisasa SGR nchini.
“Kazi ni nzuri na hizi ndio picha ambazo Watanzania wengi walikuwa na shauku ya kuziona, nimefanikiwa kuona eneo la ndani, kilichonivutia zaidi ni kuwa treni hizi zimezingatia Watu wenye ulemavu mfano katika eneo la maliwato, pia kuna eneo maalum la akina Mama kuwahudumia Watoto kwahiyo itatubadilishia namna ya kusafiri na itatoa uhuru kwa kila Mtu kusafiri, kwahiyo nimpongeze Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoahidi na kweli kazi hii inaendelea”
Aidha Balozi Mavura amesema kuwa biashara kati ya Tanzania na Korea ya kusini imeimarika zaidi kutokana na makampuni ya Nchi hiyo kuhusika katika shughuli za ujenzi wa reli na utengenezaji wa vifaa vya uendeshaji wa reli ya Kisasa “kwa kununua vifaa hivi vya uendeshaji, kiwango cha biashara kati ya Nchi zetu mbili kimepanda kwa 1.4%, tumenunua vifaa lakini pia na wao wametuuzia teknolojia”