Mwenyekiti wa ECOWAS, rais wa Nigeria Bola Tinubu amesema Jumuiya hiyo inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa demokrasia inadumishwa nchini Niger.
Ufaransa nayo kupitia kwa Waziri wake wa Mambo ya nje Catherine Colonna imelaani kwa nguvu zote hatua hiyo ya Jeshi na kutoa wito kwa ECOWAS na au kurejesha demokrasia nchini Niger.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) siku ya jana alilaani jaribio la mapinduzi nchini Niger, na kueleza kuwa ni matukio yasiyofurahisha katika uongozi wa juu zaidi wa kisiasa nchini humo.
Alionya kwamba ECOWAS “na wapenzi wote wa demokrasia duniani kote hawatavumilia hali yoyote ambayo italemaza serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya nchi.”
Bw Tinubu alisema kuwa uongozi wa ECOWAS hautakubali hatua yoyote inayozuia utendakazi mzuri wa mamlaka halali nchini Niger au sehemu yoyote ya Afrika Magharibi.
“Ningependa kusema kwamba tunafuatilia kwa karibu hali na maendeleo nchini Niger na tutafanya kila tuwezalo ili kuhakikisha demokrasia imepandwa, inakuzwa, imekita mizizi na kustawi katika eneo letu,” Bw Tinubu alisema katika taarifa aliyotia saini na ambayo hii ni kutoka jarida la premium time.
Marekani ambayo ni Mshirika wa karibu wa Niger, nayo imelaani hatua hiyo na Waziri wake wa Mambo ya nje Anthony Blinken, amekuwa na kauli hii.
‘‘Tunafuatilia kwa karibu matukio nchini Niger, nilizungumza na rais Bazuom na kumhakikishia kwamba Marekani inamuunga mkono kama rais aliyechaguliwa kihalali kule Niger.’’ amesema Anthony Blinken.