Urusi imemuweka afisa wa tatu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwenye orodha inayosakwa baada ya ICC kumshutumu Rais Vladimir Putin kwa uhalifu wa kivita nchini Ukraine, shirika la habari la serikali TASS liliripoti Alhamisi.
Jaji Tomoko Akane aliorodheshwa kama “aliyetakikana chini ya kifungu cha Sheria ya Jinai ya Shirikisho la Urusi” katika hifadhidata ya mtandaoni ya wizara ya mambo ya ndani ya Urusi, lakini bila kutaja madai yake ya uhalifu.
Mahakama ya ICC ilitoa hati za kukamatwa mwezi Machi kwa Putin na kamishna wa watoto wake, Maria Lvova-Belova, akiwatuhumu kwa kuwafukuza kinyume cha sheria mamia ya watoto kutoka Ukraine – uhalifu wa kivita.
Urusi ilijibu hati ya ICC siku tatu baadaye kwa kufungua kesi za jinai dhidi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC Karim Khan na majaji walioamuru kukamatwa kwa Putin, akiwemo Akane na Muitaliano Rosario Salvatore Aitala.
Khan na Aitala waliwekwa kwenye orodha ya wanaotafutwa na Urusi mwezi Mei na Juni mtawalia.
Akane, raia wa Japan, amehudumu kama mmoja wa majaji 18 katika ICC tangu 2018, kulingana na tovuti ya mahakama hiyo. Kabla ya hapo, alikuwa balozi wa Japan kwa ushirikiano wa kimataifa wa mahakama na pia aliwahi kuwa mwendesha mashtaka wa umma.