Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mashirika ya misaada ikiwemo jumuiya ya misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini yanatafuta ufadhili wa haraka wa kuwasafirisha watu wanaokimbia mapigano nchini Sudan.
Stephane Dujarric, msemaji mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema hayo na kuongeza kuwa: “Wengi wa wale wanaokimbia mapigano Sudan wanaishi katika mazingira magumu na hawana kifedha za kuwawezesha kuendelea na safari yao ya kukimbilia maeneo salama.”
Aidha amesema kuwa, mashirika ya misaada ya kibinadamu yamekuwa yakiwasaidia watu kufikia maeneo waliyokusudia kwa kuvuuka mito, barabara au angani lakini hayana fedha. Bila ya kuweko ufadhili mpya, mashirika hayo yatalazimika kusitisha zoezi la kuwasafirisha wakimbizi hao katika muda wa wiki mbili zijazo.
Msemaji mkuu huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesema: “Tunahitaji dola milioni 26.4 za Kimarekani kuweza kuendelea kutoa huduma hiyo hadi hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2023.”
Huku hayo yakiripotiwa, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa, idadi ya watu walioingia nchini Ethiopia kutokea Sudan inakaribia 70,000.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema hayo katika taarifa yake ya hivi karibuni kabisa na kuongeza kuwa vita vya majenerali wa kijeshi vya kuwania madaraka nchini Sudan vimewalazimisha mamia kwa maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani.
Takwimu kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la Ihamiaji zinaonyesha kuwa hadi tarehe 23 mwezi huu wa Julai, zaidi ya watu 69,000 walikuwa wamekimbilia Ethiopia kupitia vituo vingi vya mpakani katika maeneo ya Amhara, Benishangul Gumz na Gambella.
Shirika hilo nalo limelalamikia upungufu wa fedha na vitendea kazi na kusema kuwa, usafiri wa kuwafikisha wakimbizi hao kwenye maeneo waliyokusudia ni mgumu mno.