Serikali imepokea Gawio la sh. bilioni 2.5 kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Kuhifadhi Mafuta (TIPER) Tanzania, fedha hizo zitasaidia kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kupokea gawio hilo, jijini Dar es Salaam, jana, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu alisema lengo la uwekezaji wa kampuni hiyo ni kuongeza mchango kwa maendeleo ya taifa.
“Nawapongeza sana TIPER kwani walichofanya ni kiitu kikubwa, tunazihimiza kampuni nyingine kutoa gawio kwani fedha hizo ndizo ambazo zinakwenda kuinua uchumi wa nchi na kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema.
Alifafanua kuwa kuna baadhi ya kampuni ambazo mwaka ujao wa fedha zitafutwa kutokana na kupitwa na wakati au huduma zake na nyingine zitaunganishwa kutokana na shughuli zake kushabihiana ambapo zikiunganishwa na kufanya kazi pamoja zitaleta tija zaidi.
“Kuna timu inaendelea kufanya uchambuzi zaidi na mwezi wa nane mwaka huu ripoti itapokelewa na kutangazwa ni kampuni gani zitaunganishwa au kufutwa kwani wakati mwingine kampuni hufanya vibaya sababu ni uongozi hivyo lazima wapewe muda kwa kuwavumilia na kuangalia uongozi wao,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER Tanzania, Mohamed Mohamed, alisema kuwa sekta ya mafuta ni moja ya maeneo muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani na ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
“Kuwekeza katika rasilimali watu ni jambo muhimu hususan kwa kampuni ambayo inaendelea kukua na inapenda kujipqmbqnua kuwa kampuni yenye nmchango mkubwa katika jamii,” alisema.
Akizungumzia uwekezaji ambao wanataka kuufanya nchini, alisema kuwa uwekezaji umekuwa ukifanyika kipindi cha miaka 10 iliyopita na wamendelea kuwekeza, hivyo ni jambo endelevu.
Alisema TIPER imejipanga kuongeza ufanisi, ,tija na faida, na kwamba wanaimani mwaka unaokuja wanaweza kutoa gawio kubwa zaidi huenda likawa mara mbili ya walilotoa mwaka huu.