Wanachama wasiopungua 60 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameuawa katika operesheni ya pamoja ya jeshi la Somalia na vikosi vya kigeni kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wizara ya Habari ya jimbo la Kusini Magharibi nchini humo imesema katika taarifa kuwa, magaidi wa al-Shabaab wamepata pigo jingine kwa kuangamizwa wanachama wake katika operesheni hiyo mpya iliyofanyika katika mji wa El-Dhun Adegow, eneo la Bay.
Naye Kamanda wa Kikosi cha 60 cha Jeshi la Taifa la Somalia, Brigedia Jenerali Hassan Isak Omar amesema operesheni hiyo iliyojumuisha pia mashambulizi ya anga na kuangamizwa magaidi 60 wa al-Shabaab, imefanyika baina ya vijiji vya Gofguduud na Waajid.
Vyombo vya usalama vya Somalia vimesisitiza kuwa, kuondoka kwa askari wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini humo (ATMIS) hakutaathiri operesheni hizo za kukabiliana na magaidi wa al-Shabaab.
Wizara ya Habari ya Somalia ilitangaza hivi karibuni habari ya kuangamizwa magaidi wengine 100 wa al-Shabaab katika operesheni kabambe iliyofanyika wiki iliyopita katika vijiji vya Gal-Libah na El Quraq vilivyopo katika mpaka wa majimbo ya Galgaduud na Middle Shabelle, katikati ya Somalia.
Haya yanajiri siku chache baada ya watu 24, wakiwemo wanajeshi, kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia shambulio la bomu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mafungamano na al-Qaeda lenye makao yake nchini Somalia lilidai kuhusika na shambulio hilo la Jumatatu iliyopita.