MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana, amesema kuwa jukumu la kujiendeleza ni la mtu binafsi na kwamba hakuna anaeweza kumwendeleza mtu mwingine.
Amesema hata Serikali haiendelezi watu bali hujiendeleza kutengeneza mazingira mazuri kwa wananchi kujiendeleza kupitia fursa mbalimbali.
Kinana ameyasema hayo leo Julai 28, 2023 wakati akizingumza na waganga wa tiba asiili Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu ambapo pamoja na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanazofanya katika kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutengeneza mazingira mazuri na kupanua fursa za wananchi kufanya shughuli mbalimbali huku akisisitiza kuwa sasa kuba uhuru mkubwa wa watu kujieleza na kutoa maoni yao.
“Watu wanajiendeleza wenyewe, kazi ya serikali ni kutengeneza mazingira mazuri kwa wananchi kutafuta fursa wajiendeleze kama ni kilimo, kama ni biashara, kama ni ujasiriamali, kama nia ajira, kila mtu kwa nafasi yake anajiendeleza mwenyewe , hakuna mtu anayemuendeleza mwingine,” amesema.
Aliongeza kama ni biashara kubwa, tengeneza fursa nzuri za kuweza kufanyabiashara zao, ziwe za uhuru zaidi, kila inapotengeneza fursa nzuri, serikali inapotengeneza fursa nzuri watu wanakuwa na uhuru mkubwa wa kutumia akili zao, maarifa yao, na juhudi zao kujiendeleza.
“Jambo hili limekuwepo tangu Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere na ndio hivyo hivyo hadi leo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Ninyi ni mashahidi tangu Rais ameingia madarakani kazi moja kubwa aliyoifanya ni kupanua uhuru.
“Ni uhuru wa watu kufanya shughuli zao , uhuru wa kutoingiliwa , uhuru mkubwa wa kuabudu , uhuru wa kusema , uhuru wa kutoa maoni , uhuru wa kwenye makundi bila kuingilia ilimradi bila kuvunja sheria na Katiba ya Nchi.