JUMUIYA ya Khoja Shia Ithanasheri, nchini wamefanya matembezi ya kumbukizi ya siku ya Ashuraa ambayo imam Hussain (a), ambaye alikuwa mjukuu wa Mtume Muhammad (s) aliuawawa huko Karbalaa nchini Iraq mwaka 61 A.H (miaka1300 iliyopita).
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Muhammedraza Dewji alisema kuwa wanakumbuka siku hiyo kwa sababu inafundisha kuishi kwa mujibu wa maadili mema katika jamii zetu popote pale ulimwenguni.
“Dhamira yao kubwa ni kueneza maadili hayo mema yaifikie jamii ya wanadamu wote bila kujali dini zao au taifa la mtu, wanaamini kuwa mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (s) alisimama kwa ajili ya Ubinadamu na kwa Wanadamu wote na si vinginevyo , “alisema Muhammedraza.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema kuwa wanaamini hivyo kwa sababu tamaduni zote za wanadamu kwa asili zimesheheni misingi ya utu na maadili mema.
Hata hivyo, alisema kuwa kuvunjika au kupuuzwa kwa misingi hiyo katika zama hizo, ndiko kulikomfanya imam Hussain (a) alikubali kutoa maisha yake ili kuinusuru misingi hiyo ya ubinadamu duniani.
Akizungumzia sababu za kufanyika kwa matembezi hayo katika Ardhi ya Tanzania, Muhammedraza alisema kuwa Imam Hussain bin Ali (a) anasema: “Kwa hakika yeye hakutoka kwa sababu ya ujeuri wala majivuno wala kufanya ufisadi wala dhuluma, bila shaka alitoka kwa ajili ya kuurekebisha umma wa Babu yake”.
“Alitaka kuamrisha mema na kukataza maovu, yeyote mwenye kumuitikia kwa kuufuata ukweli huu, Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kustahiki mno katika ukweli na atakayempinga juu ya hilo, basi atasubiri mpaka hapo Mwenyezi Mungu, atakapohukumu kwa haki kati yake na watu hao, kwani yeye ni hakimu bora mno.” Alisema Muhammedraza.
Muhammedraza alisema kuwa huo ni ujumbe wa Imam Hussain (a) aliyoutoa wakati akiagana na ndugu yake Muhammad al Hanafiyya (r) mjini Madina, akiwa njiani kuelekea Karbalaa mnamo mwaka 60 A.H.
“Ni kauli mbiu nyepesi katika ulimi, Iakini nzito katika maana, ni wito unaopaswa kuitikiwa na kila mwenye kusikia na akatamani kuona maadili mema na utangamano katika jamii inayoongoza maisha yake” alisema Muhammedraza.
Aidha, alisema kuwa sababu za kubeba bendera katika matembezi hayo ni ishara ya huzuni kwa kifo cha Imam Hussain (a). Wakati huo huo wanaamini kuwa ni bendera za matumaini katika kuunga mkono wito wa kuamrisha mema na kukataza maovu, ili amani ipatikane ndani ya jamii ya Watanzania na duniani kote.
Matembezi hayo ni kwa ajili ya watu wote, bila kujali itikadi za kidini wala siasa, kwani msafara wa imam Hussain (a) ulihusisha Waislamu na wasiyokuwa Waislamu na wengine hawakuwa na dini kabisa Hussain (a) ni kiongozi wa watu wote.
Jumuiya ya Khoja Shia Ithanashari, ni jumuiya ya Kiislamu ambayo mbali na kutoa huduma za kiroho, pia inatoa misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa Watanzania wote, bila kujali rangi dini au kabila.
Kupitia hospitali yake ya Ebrahim Haji iliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam, jumuiya hiyo inatoa huduma bora za afya kwa bei ya chini kabisa.
Hivi karibuni jumuiya ya Khoja Shia Ithnaashri iliadhimisha kukamilika kwa miaka miwili tangu kufunguliwa kwa kituo cha afya ya macho kilichopo wilaya ya Temeke.
Huduma za macho zinazotolewa kituoni hapo ni za bei ya chini sana. Aidha kituo hiki cha Temeke kinafanya upasuaji wa mtoto jicho (cataract) bure.
Wakazi wa Wilaya ya Temeke pamoja na maeneo ya jirani ndiyo kipaumbele chao katika kuwahudumia, ingawaje huduma hii pia imewafikia wananchi wengine wanaoishi katika jiji la Dar es Salaam na pembezoni.
Jumuiya ya Khoja Shia Ithanasheri kupitia kituo ya Ebrahim Haji kinashirikiana na kikosi cha DAMU SALAMA ili kufanikisha zoezi la uchangiaji wa damu.
Ndani ya mwezi huu wa Muharram, Jumuiya ya Khoja Shia Ithnaashari inatarajia kufanya zoezi la uchangiaji wa damu kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji kuchangiwa damu salama.