Rais wa Kenya, William Ruto ametoa mwongozo mpya wa usafiri kwa Maafisa wa Serikali nchini Kenya ambapo amesema kila Afisa wa Serikali anapaswa kusafiri kwenda nje ya Nchi kwa siku 45 tu kwa mwaka na asizidishe siku hizo.
Ruto pia amesema hakuna Afisa yeyote wa Serikali anayepaswa kuwa nje ya Nchi kwa zaidi ya siku saba mfululizo huku akisema miongozo hiyo mipya ya usafiri imekuja kutokana na Maafisa wa Serikali kuwa na kiwango cha chini cha kutii maagizo kutoka kwa Mamlaka husika.
Mbali na agizo hilo, usafiri usio wa lazima bado umesitishwa na maombi yote ya usafiri yanatakiwa kufika Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora kwa ushauri.
Ruhusa za kusafiria kwa ajili ya Makatibu wote wa Baraza la Mawaziri, Makatibu Tawala Wakuu, Makatibu Wakuu, Wenyeviti na Maafisa Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Serikali yataendelea kupatikana kutoka ofisi ya Rais.
Idadi ya mahudhurio ya Mikutano na Warsha za Kimataifa itadhibitiwa pia huku Maafisa wa Serikali wakihimizwa kushiriki mikutano hiyo kwa njia za mtandao.