Rais wa serikali ya mpito ya Chad, Mahamat Idriss Déby, amesema kuwa amekutana na kuzungumza na Rais aliyeondolewa madarakani wa Niger, Mohamed Bazoum, mjini Niamey, ikiwa ni mara ya kwanza kiongozi huyo kuonekana hadharani tangu alipoondolewa madarakani na Mkuu wa Gadi ya Rais, Jenerali Abdourahmane Tchiani siku kadhaa zilizopita.
Mkutano huo ambao umefanyika kwa shabaha ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa sasa wa Niger umewajumuisha pamoja mtawala wa sasa wa kijeshi wa nchi hiyo, Jenerali Abdourahmane Tchiani na rais wa zamani wa Niger, Mohamed Issoufou.
Kwa upande wake, Issoufou amesema ataendeleza juhudi za kutafuta suluhisho la amani la mgogoro wa Niger na ametoa wito wa kuepuka vitendo vya unyanyasaji na kulinda roho na mali ya raia na wageni waliko nchini Niger.
Rais wa zamani wa Niger pia amefichua kuwa, tangu kuanza kwa mgogoro huo amekuwa akiwasiliana na pande mbalimbali kwa ajili ya kutafuta njia ya kuhakikisha Rais Bazoum anarejeshwa madarakani.
Mapema jana Jumapili, Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) iliwapa viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Niger wiki moja kumrejesha madaraka Rais Mohamed Bazoum la sivyo watakabiliwa na vikwazo, na kutishia kutumia nguvu za kijeshi dhidi yao.
Mkutano wa dharura wa ECOWAS ulioitishwa kujadili madhara ya mapinduzi ya kijeshji nchini Niger, uliamua kusitisha misaada yote ya kifedha kwa serikali ya Niamey, kusitisha shughuli za kibiashara, marufuku ya safiri kwa waliohusika na mapinduzi hayo, na kufunga mipaka na nchi hiyo.