Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Mkame Mbarawa, ametoa agizo kwa mkandarasi Sinohydro Corporation, anayejenga kipande cha pili cha barabara ya Kabingo Mnyovu Mkoani Kigoma, kufikisha mitambo eneo la kazi ndani ya siku 15 ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Mkandarasi huyo anayejenga kipande cha Kanyani Mvugwe, kilicho na urefu wa kilomita 70.5 kwa gharama ya shilingi bilioni 83.7, hadi sasa amefikia asilimia 65.30 ya ujenzi. Hata hivyo, ana muda wa miezi miwili na nusu tu kulingana na mkataba wa mradi.
Inaelezwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Kabingo Manyovu yenye urefu wa kilomita 260.1 kutakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma, ambao wamekuwa wakisubiri kufunguliwa kwa barabara hiyo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, matumaini hayo yameanza kuingia dosari kutokana na baadhi ya wakandarasi kushindwa kufuata kasi inayotakiwa katika utekelezaji wa kazi, hali ambayo imemfanya Waziri Mbarawa kutoa kauli ya Serikali baada ya kutembelea mradi huo.
Kwa wakandarasi wengine watatu wanaotekeleza mradi huo, hali inaonekana kuwa nzuri na kufikia sasa, baadhi ya maeneo tayari vipande vya barabara vimewekwa na kupitika, na wananchi wameanza kunufaika na maendeleo hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka Wakala wa Barabara nchini TANROADS kutembelea miradi inayotekelezwa ili kubaini changamoto na kuzitatua ili kuondoa sintofahamu.
Waziri Profesa Mkame Mbarawa ametembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo Manyovu wenye urefu wa kilomita 260.1, unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 360.5, ambao kwa mujibu wa mkataba unatakiwa kukamilika mwaka huu kwa vipande vyote vinne.