Ni Agosti 1, 2023 ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya za mafuta ambazo zinaonesha Petroli imepanda kwa shilingi 443 huku Dizeli ikipanda kwa shilingi 391 kwa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa bei mpya zilizotangazwa leo na EWURA, Petroli iliyokuwa inauzwa shilingi 2,736 imepanda hadi kufikia shilingi 3,199 huku Dezeli iliyokuwa inauzwa shilingi 2,544 imepanda hadi 2,935, kwa Dar es Salaam bei ambazo zitaanza kutumika kesho Jumatano, Agosti 02,2023 saa 6:01 usiku.
Aidha EWURA imesema sababu za mabadiliko ya bei hizo kwa mwezi Agosti 2023 ni changamoto za upatikanaji wa Dola za Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani, ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa mafuta.
Imesema kwa mwezi Agosti 2023, bei za rejareja za mafuta katika Mikoa ya Tanga yatauzwa sh. 3,245 na Mtwara ni sh. 3,271.