Walimu mkoani Njombe wameendelea kuweka msimamo wa kugoma kuingia kwenye mchakato wa Uchaguzi ili kujaza nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji taifa (KUT) kutoka kwenye Mkoa huo mara baada ya kufutwa Uanachama aliyekuwa Mjumbe wa nafasi hiyo.
Wajumbe wa Kamati tendaji Wilaya ya Njombe wameonyesha msimamo huo wakati wakizungumza na vyombo vya habari ikiwa ni siku chache zimepita tangu msimamo huo ulipowekwa wazi na wajumbe wengine wa wilaya za Ludewa na Wanging’ombe wakidai kuwa hawaoni sababu ya kuingia katika uchaguzi kwa kuamini kuwa wajumbe 18 wa kutoka mikoa mbalimbali akiwemo mjumbe wao Thobias Sangawaliondolewa kimakosa.
Mwenyekiti wa chama cha walimu (CWT) Wilaya ya Njombe Valien Ngalyoma amesema chama hicho kilipokea barua yenye kumbukumbu namba AB 277/320/10/100 ya June 22 mwaka huu 2023 kutoka kwa katibu wa CWT Taifa ambayo pamoja na maazimio mengine ilikuwa na azimio la kuwafuta uanachama wajumbe 20 ambao kati yao wajumbe 18 ni wakamati ya utendaji taifa.
Amesema kamati tendaji ya Wilaya hiyo imeazimia mambo kadhaa ikiwemo kuto tambua maamuzi ya baraza la taifa ya kumvua uanachama Thobias Sanga kwa kuwa walimu wa Njombe hawajawahi kufanya mchakato wowote wa kumvua uanachama.
“Azimio la pili ni kuwa kamati ya utendaji ya chama cha walimu wilaya ya Njombe haitashiriki uchaguzi wowote unaohusiana na kuziba nafasi ya KUT kwani KUT wa Njombe Thobias Sanga tunamuamini na anatufaa na tupo naye kwa kila hatua kuahakikisha kazi tuliyomtuma anaifanya”amesema Ngalyoma
Aidha kamati hiyo imeazimia kumchukulia hatua kiongozi yeyeote wa chama ngazi ya wilaya amabye ataonekana kuunga mkono na kufurahia azimio la hovyo la baraza la taifa kwa kuwa wote tumesoma katiba na kujiridhisha kuwa KUT 18 walifutwa uanachama kienyeji kwa miemko ya viongozi wa kitaifa.
Mwalimu Philipo Ndimbo ni muwakilishi wa walimu wenye ulemavu wilaya ya Njombe amebainisha kuwa kutokana na migogoro iliyopo kwa viongozi mambo mbalimbali yameendelea kukwama kinyume na matakwa ya katiba huku Mwalimu Magdalena Kisonga ambaye ni muwakilishi wa CWT mahali pa kazi akieleza kuwa wanachama wamevunjika mioyo ya kuendelea kuwa wanachama na kuwataka viongozi kukaa na kumaliza migogoro yao.
Miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha kufutwa uanachama wajumbe hao ni pamoja na kufanya kikao miezi kadhaa iliyopita na kuweka maazimio ya kumkasimisha madaraka naibu katibu mkuu ya katibu mkuu kwa madai kuwa ilionekana katibu mkuu alikuwa akifanya kazi kinyume na katiba.